Tabia Na Shida Katika Huduma

Hope for Today (Swahili)
Hope for Today (Swahili)
Tabia Na Shida Katika Huduma
/
II Wakorintho 4:1-18

Hujambo msikilizaji. Natumai u buheri wa afya na ni furaha yetu kukuletea kipindi hiki cha matumaini. Leo twalitazama fungu la Neno la Mungu kutoka 2 Wakorintho 4:1-18.

Jina langu ni David Mungai. Wimbo halafu tuendelee.

Naam na Karibu tujifunze Neno kutoka 2 Wakorintho 4:1-18 “TABIA NA SHIDA KATIKA HUDUMA” nakuomba usikilize kwa makini na ukiwa na swali, Anwani na nambari ya simu tutakusomea tumalizapo somo, Karibu. Twalichambua fungu la Neno kutoka 2 Wakorintho 4:1-18. Tutaligawa mara mbili (1) 1-6

Mwanga wa Injili (2) 7-18 Hazina katika vyombo vya udongo. Kwanza nasoma mstari wa 1-18. 2 Wakorintho 4:1-18.
1 kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatutegei.

2 Lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya Neno la Mungu na uongo bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za Mungu,

3 Lakini ikiwa Injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea

4 ambao ndani yao mungu wa Dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.

5 kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo, ya kuwa ni Bwana, na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Injili ya Yesu.

6 kwa kuwa Mungu, aliyesema, nuru itang’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo

Katika fungu hili, Paulo atuonyesha ya kwamba, Injili ni nuru na mna rehema ndani ya Injili, na kwa hiyo katika mstari wa pili, Paulo kwa nguvu asema “…tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya Neno la Mungu na uongo…”

Hayo yote, kama yalivyokuwa korintho, ndivyo yalivyo hapa kwetu, kwa sababu ya faida ya kibinafsi, uongo, ushirikina, wivu, mgawanyiko hata vita vya kimwili. Sharika zingine zimekuwa uwanja wa vita vya maneno na vitendo. Paulo atukumbusha ya kwamba , Injili ya Bwana wetu Yesu Kristo ni Kuleta nuru na mwanga, maishani, rohoni na moyoni. Naomba tuache kabisa hiyo tabia.

Fungu au sehemu ya pili. Mstari wa 7-18. Hazina katika vyombo vya udongo. Nasoma;

7 Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwenu.

8 pande zote twadhihikika, bali hatusongwi, twaona shaka, bali hatukati tamaa,

9 twaudhiwa , bali hatuachwi, twatupwa chini bali hatuangamizwi,

10 siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.

11 kwa maana sisi tulio hai siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti

12 basi hapo mauti hufanya kazi ndani yenu.

13 Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani, kama ilivyoandikwa. Naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena, sisi nasi twaamini na kwa sababu hiyo twanena,

14 tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi, nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi.

15 kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.

16 kwa hiyo hatulegei ( kama mstari wa kwanza. Hatulegei) bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.

17 maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kwa mwingi sana

18 tusiviangalie vinavyoonekana bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu, bali visivyoonekana ni vya milele

Sisi ni kama vyombo vya udongo, Lakini Mungu, ametubebesha dhahabu- hazina ya Injili, iletao uhuisho.

Tusichoke mpaka Kristo arudi.

Pamoja na hayo, hata tunapoteswa, hatuwezi kuyalinganisha na yalio Mbinguni kama anavyosema katika Warumi 8:18.
“kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu.”

Mateso ya wakati huu ni ya muda mfupi tu, utukufu watungojea Mbinguni.