Wote Waajibike (Mume Na Mke)

Hope for Today (Swahili)
Hope for Today (Swahili)
Wote Waajibike (Mume Na Mke)
/
I Wakorintho 7:10-16

Hujambo msikilizaji wangu mpendwa popote ulipo na karibu tujifunze Neno pamoja. 1 Wakor 7:10-16 “Sote tuwajibike.” Jina langu ni David Mungai. Karibu wimbo halafu tuendelee.

WIMBO

Naam. Karibu tena, tujifunze Neno la Mungu. 1 Wakor 7:10-16. Mungu aliiangamiza dunia wakati wa Nuhu kwa sababu wanadamu walishindwa kukabiliana na tamaa za kuonana kwa mume na mke. Ikawa wanayafanya mapenzi kiholela holela, ikawa afadhali Wanyama wa porini. Nasoma mwanzo 6:1-2.

“Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao. 2. Wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri, wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.

Bwana wetu Yesu Kristo pia, katika Injili ya Mathayo 24:36-37, alitoa unabii akasema, “36 Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake. 37 Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.”

Nyakati hizi zetu, zimekuwa zaidi ya wakati wa Nuhu. Uzinzi na usherati umezidi. Talaka na ndoa kuvunjika ni hadithi za kila siku. Mipango ya kando ni tele, nao wengi wametuacha kwa sababu ya maradhi yasiyokuwa na tiba. Mtume Paulo, kwa uongozi wa Rojho mtakatifu aliandika 1 Walkor 7:10-16 maneno ndiyo haya.

10 Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe;

11 lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.

12 Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache.

13 Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.

14 Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu.

15 Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani.

16 Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo?

Kwanza kabisa, kutoka kwa fungu hili twapata ukweli kwamba Mst 10. “Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza, wala hapo si mimi, ila bwana, mke asiachane na mumewe.” Hiyo ni amri. Iwapo hutaki kufungwa pingu za Maisha basi, usioe au usiolewe. Ukioa, kaa na uishi hivyo. Ukiolewa, ni vivyo hivyo.
Jambo la pili. Ni ushauri. Mst 11-14.

11 lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.

12 Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache.

13 Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.

14 Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu.

Paulo atafuta amani kati ya mume na mke. Kama hujaoa, Ni vyema kujua vile Neno lasema na kufundisha hivi.

2 Wakor 6:14:

14 Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?

Iwapo ushaoa na mwenzako Mkristo, Paulo apendekeza muishi kwa furaha na kuelewana, bila unafiki, asieamini akikataa basi na aende lakini kwa amani, ukikumbuka maneno ya Mst 16

“Kwa maana wajuaje wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje wewe mwanamume kama utamwokoa mkeo?”

Ndoa ni ukweli usiobadilishwa, na mtu au kitu cho chote. Mkishaoana, ombeni. Mungu awasaidie kuishi pamoja kama vile kanisa lilivyo pamoja na Yesu Kristo. Tupalilie uhusiano wetu, tuishi kwa amani maishani mwa ndoa. Tukingojea kwa hamu siku ya kurudi kwake Yesu. Kanisa lijirebeshe kama Bi harusi.

Tujifunze kutubu na kuungama dhambi ili Kristo akirudi atukute tayari tumetakaswa na kutakatishwa.