Tenda Yaliyo Haki

Hope for Today (Swahili)
Hope for Today (Swahili)
Tenda Yaliyo Haki
/
Danieli 1:8-21

Hujambo na karibu, tujifunze neno la Mungu pamoja. Leo twaanza mfululizo wa masomo kutoka kitabu cha Nabii Danieli. Katika kitabu hiki Danieli atufunza namna ya kutenda yaliyo haki. Jina langu ni David Mungai wimbo halafu tuendelee.

WIMBO

Karibu tena tujifunze neno kutoka kitabu cha Danieli.

Jina Danieli maana yake ni ‘Mungu ndiye hakimu wangu.’ Danieli alifanya kazi katika nyumba za wenye mamlaka nchini Babeli. Alichukuliwa kama mtumwa nchini Babeli, na Nebukadinezaru mnamo mwaka wa 605 kabla ya kuzaliwa Kristo. Katika miaka iliyofuata alitumika katika serikali ya Babeli kwa muda mrefu lakini hakusahau huduma yake kama nabii wa Mwenyezi Mungu.

Danieli, ndiye mwandishi wa kitabu hiki, kama tunavyosoma katika sura ya 12:4.

“Lakini wewe, Ee Danieli, yatunge maneno haya ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka.”

Bwana wetu Yesu Kristo, katika injili ya Mathayo 24:15, alimtambua Danieli kama Nabii. Nasoma Matt 24:15

“Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na Nabii Danieli, limesimama katika patakatifu(asomaye na afahamu).”

Na kwa sababu Danieli hakuketi katika afisi ya Nabii, kitabu hiki kimewekwa “maandishi” katika Bibilia ya Kiebrania badala ya kuwekwa pamoja na vitabu vya manabii, lakini maishani mwake Danieli, alisimama wima na mtumishi wa Mungu mwaminifu.

Baada ya utangulizi huo sasa nasoma kitabu cha Danieli 1:8-21.

8 Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme wala kwa divai aliyokunywa, basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi.

9 Basi Mungu alimjalia Danieli kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi.

10 Mkuu wa matowashi akamwambia Danieli, mimi namwogopa bwana wangu, mfalme, aliyewaagizia nyinyi chakula chenu na kinywaji chenu, kwa nini azione nyuso zenu kuwa hazipendezi kama nyuso za vijana hirimu zenu? Basi kwa kufanya hivyo mtahatarisha kichwa change mbele ya mfalme.

11 Ndipo Danieli akamwambia yule msimamizi, ambaye mkuu wa matowashi amemweka juu ya Danieli na Hanania, na Misheki na Azaria.

12 Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi na watupe mtama tule, na maji tunywe.

13 Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za wale vijana wanaokula chakula cha mfalme; ukatutendee sisi watumishi wako kadiri ya utakavyoona.

14 Basi akawasikiliza katika jambo hilo, akawajaribu siku kumi.

15 Hata mwisho wa zile siku kumi nyuso zao zilikuwa nzuri Zaidi na miili yao ilikuwa imenenepa Zaidi kuliko wale vijana wote waliokula chakula cha mfalme.

16 Basi yule msimamizi akaiondoa posho yao ya chakula, na ile divai waliyopewa wanywe, akawapa mtama tu.

17 Basi kwa habari za hao vijana wane, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote na ndoto.

18 Hata mwisho wa siku zile alizozoagiza mfalme za kuwaingiza, mkuu wa matowashi akawaingiza mbele ya mfalme Nebukadneza.

19 Naye mfalme akazungumza nao, na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria, kwa hiyo wakasimama mbele ya mfalme.

20 Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaaa mara kumi Zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake.

21 Tena, Danieli huyo akadumu huko hata mwaka wa kwanza wa mfalme Koreshi(Cyrus).

Vitendo vyetu maishani vyaonyesha tu watu aina gani hata anavyotembea mtu huonyesha tabia zake. Maisha na vitendo vya Danieli ni changamoto kubwa kwetu.

Twaona wazi ya kwamba, Danieli kama mcha Mungu, moyoni mwake aliamua kwamba hatakula wala kunywa chochote kingaliuchafua moyo na mwili wake. Uhusiano wake na Mungu ulikuwa muhimu kuliko chakula na vinywaji. Uhusiano wetu na Mungu ni muhimu kuliko vyote vya duniani. Vya duniani na vya kimwili vitaisha, vitafika kikomo, lakini baada ya maisha haya tunayo maisha au uzima wa milele mbinguni. Na tunapojitoa kwake Mungu, Mungu naye, kama alivyomtendea Danieli atatutendea pia.

Uzima wa milele, pamoja na Kristo ni bora na muhimu kuliko chakula na raha za duniani hii. Tusiichafue miili yetu kama makao ya Roho Mtakatifu kuwa deni la machafu yote ya dunia hii.

Ni muhimu kusimama wima kama Wakristo tukikumbuka ya kwamba, kitambo kurudi kwake Yesu Kristo. Sisi ndiyo mawakili, mabalozi wake Mungu, kama Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria na Abednego katika nchi ya utumwa “Babeli.”

Naomba tuwe hivyo duniani.