Namna Ya Kutoa Uamzi Wa Maana

hft swahili 2022
Hope for Today (Swahili)
Namna Ya Kutoa Uamzi Wa Maana
Loading
/
I Wakorintho 10:23-33

Hujambo. Natumai u buheri wa Afya na karibu tujifunze Neno pamoja. Leo twalichambua fungu la Neno kutoka 1 Wakorintho 10: 23-33. “NAMNA YA KUTOA UAMUZI WA MAANA.” Jina langu ni David Mungai.

Karibu wimbo, halafu tuendelee.

Naam. Karibu tena. Sisi Wakristo, ni muhimu tujue namna ya kutoa uamzi wa maana, katika Maisha yetu. Kutoka kwa 1 Wakorintho 10: 23-33, twapata mambo kadhaa ya busara kutusaidia kuamua kwa busara.

Nasoma fungu hili la Neno sasa.

1 Wakorintho 10:23-33:

23 Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo.

24 Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya mwenzake.

25 Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni, bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri;

26 maana, Dunia ni mali ya Bwana na vyote viijazavyo.

27 Na mtu asiyeamini akiwaalika, nanyi mnataka kwenda, kuleni kila kitu kiwekwacho mbele yenu bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri.

28 Lakini mtu akiwaambia, Kitu hiki kimetolewa kiwe sadaka, msile, kwa ajili yake yeye aliyeonyesha, na kwa ajili ya dhamiri.

29 Nasema, dhamiri, lakini si yako, bali ya yule mwingine. Maana kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine?

30 Ikiwa mimi natumia sehemu yangu kwa shukrani, kwa nini nitukanwe, kwa ajili ya kitu nikishukuriacho?

31 Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.

32 Msiwakoseshe Wayahudi wala Wayunani wala kanisa la Mungu,

33 vile vile kama mimi niwapendezavyo watu wote katika mambo yote, nisitake faida yangu mwenyewe, ila faida yao walio wengi, wapate kuokolewa.

Maneno ya mstari wa 31 yatoa ushauri kwamba tufanye yote kwa utukufu wa Mungu. Hii ndiyo kanuni na wito wetu. Ushauri huu ulianza kutoka 1 Wakor 8:1, “Na kwa habari ya vituvilivyotolewa sadaka kwa sanamu, Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga. Kwa hivyo, ni vizuri kuyafikiri na kuyatenda yanayotujenga sisi na kanisa lake Kristo.

Lakini twawezaje kujipima au twawezaje kujua kama twatoa uamzi, unaolingana na mapenzi ya Mung una kwa utukufu wake? Tutazame maneno ya 1 Wakor. 6:12.

“Vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu chochote.”

Kwa hiyo, katika uamzi uwao wote, jifunze kujiuliza maswali haya.

1) Je, uamzi huu una faida gani kwangu binafsi au katika kanisa la Mungu?

2) Je, uamzi huu utanifanya mtumwa? Kwa mfano, unapoanza kunywa pombe kidogo, kidogo, kuna uwezekano siku moja utalewa pombe. Ulianza kidogo kidogo na hatimaye utaishia kuwa mlevi wa kupindukia. Kila dhambi au tabia huanza pole pole kidogo kidogo. Hatimaye yamfanya mtu mtumwa.

3) Swali. Je uamzi huo utakuwa kikwazo katika kukua kwangu kiroho? Je, uamzi wako utamkwaza ndugu au dada katika Kristo?

Tazama maneno ya 1 Wakorintho 8:13. “Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu.”

4) Je, uamzi wako, utakujenga, na kanisa la Bwana?
1 Wakorintho 10:23 “Vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu chochote.”

Kwa kifupi tujifunze kujiuiza, “Kristo na mapenzi yake wako wapi katika uamzi huu wangu?” Kuwa macho usije ukatubukizwa katika uamuzi mmbaya usije ukajuta baadaye.

Receive Weekly Encouragement

Sign-up to get a sermon straight to your inbox on a weekly basis!